Na Elias Mhegera
Mjadala mkubwa unaoendelea nchini Tanzania kwa sasa ni kuhusu yaliyojiri kuhusiana na ‘mchanga’ wa dhahabu au ‘makinikia’ na pia athari zake baadaye kisiasa na kisheria pia.
Watanzania wamechachamaa kwa hamasa kubwa, wakiwashambulia wabunge wao kwa kuruhusu mambo ya aina hii yaendelee kwa muda mrefu kwa sababu za kulindana na kutumia wingi wa wale waliokuwa wanaunga mkono.
Wadau mbali mbali wanapendekeza kwamba mikataba yote ya madini ijadiliwe upya. Lakini pia wanataka sheria za mikataba zizingatiwe ili taifa ingie matatani na wawekezaji
Wananchi kwa ujumla wanaona kwamba kuna miswaada ilipitishwa kwa hati ya dharura ka malengo mabaya. Na haya yote yaliwezekana kwa sababu ya mfumo mbovu wa kisiasa.
Mjadala wa jambo hili ni mpana ipo ya kisheria, na kisiasa pia. Prof. Abdallah Safari ambaye ni wakili wa kujitegemea pamoja na kwamba yeye pia ni makamu mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) anasema hili ni janga jingine.
Anaiona hofu kwamba uamuzi uliochukuliwa hata kama una manufaa kisiasa lakini unaweza kuwa na athari za kisheria. Sababu kubwa ni kwamba mikataba hii ilifikiwa kwa maridhiano ya pande mbili.
Na kwa maana hiyo pande hizo zinaweza kuirejea mikataba hiyo na kuangalia wapi pa kurekebishwa. Anahofu kwamba upo uwezekano kwamba wawekezaji wakienda mahakamani yanaweza kujitokeza yale yale ya ile kesi ya ‘samaki wa Magufuli’ kama ilivyotambulishwa wakati ule.
Anasema Tanzania inayo bahati kwamba ipo sheria ya mikataba inayoheshimika kimataifa inayoitwa “The Nyerere Doctrine of State Succession” ambayo ilihusu mikataba iliyokuwapo wakati wa uhuru na mabadiliko yaliyotakiwa kufanyika baada ya nchi kupata uhuru.
Prof. Safari anasema kwamba ameongea na wakili Ibrahim Bendera aliyekuwa wakili wa walalamikaji katika kesi ya meli na wakili huyo anasema kwamba mwisho wa jambo hili ni kufikishwa kwenye mahakama za kimataifa na serikali yetu inaweza kuingia matatani.
Wakili maarufu wa kujitegemea jijini Mwanza Bw. James Njelwa ambaye pia amewahi kufanya kazi na asasi ya sheria za mazingira (LEAT) anasema kwamba huwezi kusema tu kwamba sheria imevunjwa bila kuwa umeusoma mkataba wenyewe ulikuwa na vipengele gani.
Hata hivyo hofu yake ni kwamba iwapo mliingia mkataba na mwenzako huwezi kuuvunja mkataba huo kwa kutumia jeshi la Polisi au kwenda na vyombo vya habari katika kuuvunja.
Hofu yake ni kwamba wawekezaji wanaweza kujiona kwamba labda walidhalilishwa kwa mambo hayo kuhusisha sana vyombo vya habari.
Kimsingi mikataba hiyo ilifikiwa chini ya utawala wa awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa. Hofu ni kwamba ripoti ya Prof. Abdulkarim Mruma itaibua mambo mengi ya tokea 1998 nchi ilipoingia mikataba hii.
Na kwa mana hiyo wapo wanaoona kwamba Prof. Sospeter Muhongo hakustahili kubebeshwa mzigo wa lawama yeye peke yake na watendeji wengine walioadhibiwa bali hata marais wastaafu Mkapa na Jakaya kikwete.
Wadau wanaona sheria zilikuwa zinampa wakati mgumu Prof. Muhongo kufanya lolote ila kutii alichokikuta kwa lengo la kuilinda nafasi yake ya uwaziri.
Kamati ya Mh Rais iliyokuwa chini ya Prof Mruma inasema nchi ya Tanzania imeibiwa sana. Lakini mwekezaji(Acacia) anasema ripoti hiyo imeongopa,haijatoa takwimu za ukweli.
Mwanasheria mkuu wa serikali wa zamani Andrew Chenge amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa kamati ya Rais iliyoongozwa na Prof Mruma, imeongopa kwa kutoa taarifa isiyo sahihi.
Ni mazingira hayo yanayoleta sintofahamu ya kisaa na kisheria pia. Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete na Rais John Magufuli wote wamefanya kazi katika awamu hizo mbili. Kulingana na utamaduni wa kiutendaji serikalini yapo mambo ambayo viongozi waliotangulia na waliopo madarakani wanaweza kuyamaliza kimya kimya.
Jambo hilo linawezekana zaidi kwa serikali iliyoongozwa na chama kimoja kwa muda wote kama ilivyo kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Mkataba huu mmoja unaopigiwa kelele sasa ni miongoni mwa mikataba mingi iliyowahusu viongozi wa kitaifa hususani rais mwenye dhamana kuu ya fedha za serikali yaani “sovereign bond”.
Mkataba huu ni mmoja wa viashiria vya matumizi mabaya ya dhamana kwa malengo ya kujipatia utajiri kwa watu binafsi, kikundi cha watu na hata labda chama tawala chenyewe CCM.
Kwa mantiki hiyo uamuzi huu unampa heshima kubwa mtu binafsi ambaye ni rais wa sasa na kwa wakati huo huo unawavunjia heshima watangulizi wake wawili Mzee Mkapa na mwenzake Kikwete.
Ni vigumu sasa kubashiri athari za muda mrefu za kisiasa za jambo hili yaani mpambano wa kujijengea kuheshimika ‘fight of legacies’. Hata hivyo zinakidhi mahitaji ya sasa ya kisiasa.
Ni kweli kwamba yanayofanywa na Rais Magufuli ni kiashiria cha uzalendo, lakini ni vyema pia kuwa na mkakati wa kuondosha ufisadi na uoza nchini bila kuvunja sheria. Wizi katika sekta ya madini haukuanza leo, na hata kelele dhidi ya wizi huo hazijaanza leo. Kujiuzulu au kuondolewa kwa waziri wa nishati na madini hakujaanza leo.
Ni vyema kuja na mkakati wa kudumu wa kushughulikia suala hilo ‘comprehensive approach’ badala ya kuangalia leo bila kukumbuka kesho nini kinaweza kutokea.
Kivita unaweza kusema Prof. Muhongo ni ‘cross fire victim’ yaani risasi zinarushwa kutoka upande mmoja kwenda mwingine na mtu asiyevifahamu vizuri vita hivyo anajikuta kapigwa risasi.
Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 CCM ilimuuza ‘mtu binafsi’ Magufuli kwa sababu chama kilihofu kwamba hakiuziki, kwa sasa mtu huyo anataka kuhalalisha kwa Watanzania kwamba kweli alistahili kuwa rais wa nchi na anayo mapenzi ya dhati kwa nchi na watu wake.
Ni vigumu kwa watendaji walioko serikalini kufahamu wanatakiwa wafanye nini katika mazingira ya sasa wakati rais wa nchi amelenga kujenga utamaduni mpya. Mawaziri na watendaji wengine wanafahamu kwamba ili kulinda ajira yako ni lazima ufuate kanuni za mfumo wa serikali ulioukuta.
Muhongo aliteuliwa na wanasiasa wanaoujua mfumo kuliko yeye ambaye muda mwingi alikuwa vyuoni na labda hata akiwa nje ya nchi. Kwake ilibidi ajue ajipange vipi ili aweze kukidhi mahitaji ya mfumo wa sasa bila kuwakera watangulizi ambao hasa ndiyo walianza kumuamini na kumkabidhi wadhifa.
Na kwa mantiki hiyo Prof. Muhongo na hata wenzake waliodhibiwa amehukumiwa kwa kubeba dhambi ya watu wengine ambazo hata rais wa sasa alipata kuzibeba kwa kile kinachoitwa ‘collective responsibility’ yaani uwajibikaji wa pamoja akiwa ndani ya awamu hizo.
Pamoja na kumpongeza Rais Magufuli kwa hatua zake madhubiti ni vyema pia akazikumbuka sheria za kimataifa ili taifa lisije kuingia matatani mbele ya safari. Tuwasiliane: mhegera@gmail.com Simu 0715-076272 Pichani: Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju
Maoni
Chapisha Maoni