Mikopo
kwenye viwanda, kilimo yaporomoka
Wakati serikali ikijipanga kuifanya Tanzania kuwa nchi ya
viwanda, kiwango cha mikopo kwenda kwenye sekta hiyo, pamoja na kilimo
imeporomoka katika kipindi kilichoishia Juni mwaka huu, ikilinganishwa na
kipindi kinanchoishia Juni mwaka jana.
Kwa mujibu wa ripoti ya mapitio ya uchumi ya mwezi Julai
mwaka huu iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT)kushuka kwa kiwango cha
mikopo pia ilizikumba sekta nyingine za uchumi.
Sekta nyingine zilizokubwa na kuporomoka kwa kiwango cha mikopo
ni biashara, usafiri na mawasiliano pamoja na ujenzi na majengo.
Ripoti hiyo imeonyesha kwamba mikopo kwenda kwenye sekta
ya viwanda imeporomoka hadi kufikia -4.6 mwezi Juni mwaka huu kutoka asilimia
26.3 ya mikopo yote mwezi Juni mwaka jana.
Mikopo kwenda kwenye kilimo, sekta ambayo inaajiri
watanzania wengi hasa wale wa vijijini, nayo imeshuka hadi kufikia asilimia
-0.1 mwezi Juni 2016 kutoka asilimia 7.6 Juni mwaka jana.
Ripoti kutoka sekta ya benki pia imeonyesha kwamba kiwango
cha mikopo kwenye sekta ya biashara, ambacho Juni mwaka jana ilikuwa ni
asilimia 27.3 ya mikopo yote, iliporomoka hadi kufikia asilimia 3.5 Juni mwaka
huu.
Sekta ya usafiri na mawasiliano nayo pia ilikumbwa na
kuporomoka kwa kiwango cha mikopo ambapo ripoti imeonyesha kwamba imeporomoka
hadi kufikia asilimia 8.5 mwezi Juni mwaka huu.
Mikopo kwenda kwenye sekta ya ujenzi na majengo nayo
ilishuka hadi kufikia asilimia 10 ya mikopo yote mwezi Juni mwaka huu kutoka
asilimia 13.2 mwezi Juni mwaka jana.
Hata hivyo, ripoti hiyo imeonyesha kwamba mikopo kwenda
sekta hiyo iliongezeka katika kipindi cha mwezi mmoja kutoka asilimia 3.7 mwezi
Mei hadi asilimia 10 mwezi Juni mwaka huu.
BOT imesema kwenye ripoti hiyo kwamba kupungua kwa mikopo
kwenye sekta mbalimbali za uchumi inatokana na sekta ya benki na sekta binafsi
kuangalia muelekeo wa sera za uchumi za serikali ya awamu ya tano.
Hata hivyo, pamoja na kupungua kwa mikopo kwenye sekta
hizo, mikopo ya wafanyakazi wenye mishahara pamoja na ile ya hoteli na migahawa
iliongezeka katika kipindi hicho.
Ripoti hiyo imeonyesha kwamba mikopo ya hoteli na
migahawa kwa kipindi cha mwaka ulioishia Juni mwaka huu ilikuwa ni asilimia 18
kutoka asilimia 10 mwezi June mwaka jana.
Kwa upande wa mikopo ya wafanyakazi wenye mishahara,
kiwango chake kiliongezeka hadi kufikia asilimia 36.7 ya mikopo yote mwezi Juni
mwaka huu kutoka asilimia 22.1 mwezi Juni mwaka jana.
.
Maoni
Chapisha Maoni