Swissport, TCC zaongoza kuzafanya vizuri Afrika
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI za Sigara Tanzania (TCC) na ile inayotoa huduma za usafiri wa anga nchini ya Swissport ni miongoni mwa kampuni 25 zinazofanya vizuri barani Afrika.
Kwa mujibu wa jarida la Global Finance kampuni hizo ndizo pekee kwenye ukanda wa Afrika Mashariki  (EAC) zilizoorodheshwa kufanya vizuri kwa mwaka 2015.
Swissport na TCC zote zimeorodheshwa kwenye soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) na kwa mujibu wa ripoti za soko, kampuni hizo pia ni miongoni mwa kampuni zinazofanya vizuri.
Kampuni hizo pia zimeshika nafasi ya pili kisekta kila moja ambapo Swissport ni kwa upande wa usafiri na TCC kwa upande wa uuzaji wa bidhaa jumla na rejareja.
Ripoti hiyo ambayo ni kwa ajili ya kampuni zilizoorodheshwa kwenye masoko ya hisa iliangalia vigezo mbalimbali ikiwemo hali ya ukwasi (liquidity), pato toka kwenye rasilimali na kiwango cha faida inayopatikana kutoka kwenye uwekezaji.
Kwa mujibu wa jarida hilo, Swissport imeshika nafasi ya nne huku Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) ikishika nafasi ya 17.
Kwa upande wa vigezo, ripoti hiyo inaonyesha kwamba ukwasi wa kampuni ya Swissport  ni asilimia 2.67, pato la rasilimali ni asilimia 46.54 wakati faida ni asilimia 42.06. Swissport ilipanda alama za jumla 67.
Pamoja na kushika nafasi ya nne kwenye orodha ya jumla, Swissport, ambayo ni miongoni mwa kampuni tanzu za Swissport International imeshika nafasi ya kwanza miongoni mwa kampuni zote 25 kwa kuwa na kiwango kikubwa cha pato toka kwenye rasilimali ambalo ni asilimia 46.54 zaidi ya asilimia 20.24 ya kampuni iliyoongoza..
Ukwasi wa kampuni ya TCC  ni asilimia 1.14 wakati pato toka kwenye rasilimali ni asilimia 27.72 na faida ni asilimia 34.06. Kwa ujumla TCC ilipata alama 138 zilizoifanya ishike nafasi ya 17.
Ripoti hiyo imeonyesha kwamba kampuni zilizofanya vizuri kwenye orodha hiyo ni zile za Afrika Kusini ambazo ni kumi, zikifuatiwa na Misri ambayo kampuni zake ambazo ni tisa.
Kwa mujibu wa ripoti za soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) bei ya hisa za Swissport ziliongezeka na kufikia shilingi 7,350 Desemba 31 mwaka jana kutoka shilingi 5,240 mwezi Januari mwaka jana.
Hata hivyo, kwa mwaka jana bei ya hisa za TCC ilishuka hadi kufikia shilingi 15,950 mwisho wa mwezi Desemba, kutoka shilingi 17,100 mwezi Februari.
Nchi nyingine za Afrika ambazo kampuni zake zimetajwa miongoni mwa kampuni 25 zilizofanya vizuri ni Morocco ambayo imetoa kampuni tatu na Zimbabwe ikitoa kampuni moja.
Kampuni iliyoongoza kwenye orodha ni Alexandria Container and Cargo ambayo ina ukwasi wa asilimia 6 wakati pato la rasilimali ni asilimia 20.24 na  kiwango cha faida ni asilimia 59.31. Kampuni hii ilipata alama za jumla 13 na kuifanya kuongoza.
Kampuni ya pili ni Compagnie Miniere De Touissit kutoka Morocco ambayo ukwasi wake ni asilimia 4.27 na faida toka kwenye rasilimali ni asilimia 20.24, kiwango cha faida ni asilimia 49.37 na ilipata alama ya jumla 46.
Kwa upande wa kisekta, Kampuni ya Phoenix Beverages ya Mauritius ndiyo iliyoongoza kwenye sekta ya chakula, vivywaji baridi na tumbaku , Tunisia Air Liquide Tunisie ikaongoza kwa upande wa gesi, maji na umeme na Spur Corporation ya Afrika Kusini ikaongoza kwenye sekta ya hoteli na migahawa.
Mwisho




Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Tanzania intra-SADC trade decline by 15 pc

DSE all share index down

The beauty queen from Tanzania who is building a furniture empire